Thursday, September 15, 2011

Kamati ya Tibaigana Sept. 24


Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakutana tena Septemba 24 mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza mashauri matatu dhidi ya Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage na Ofisa Habari wa klabu ya Yanga, Louis Sendeu.

Awali kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alfred Tibaigana ilikuwa ikutane Agosti 29 mwaka huu kusikiliza malalamiko ya TFF dhidi ya viongozi hao, lakini kikao kiliahirishwa kutokana na Kamati kutotimiza akidi (column) kwa wajumbe wake.

Pia TFF imewasilisha kwa kamati hiyo shauri jipya dhidi ya Sendeu kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi aliyechezesha mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Sendeu alimshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao, na anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba na kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima haikuwa halali.

No comments:

Post a Comment