Thursday, September 15, 2011

Iniesta nje Mwezi Mmoja


Klabu ya Barcelona imetangaza kwenye mtandao wake kwamba, Andres Iniesta atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja.

Kiungo huyo aliumia dakika 5 kabla ya mapumziko, kwenye mechi ambayo timu yake ilitoka sare ya 2-2 na AC Milan, katika michuano ya Kombe la mabingwa Barani Ulaya siku ya Jumanne.

Iniesta atakosa mechi dhidi ya Osasuna, Valencia, Atletico Madrid, BATE Borisov na Sporting Gijon.

Mchezaji huyo anategemea kurudi tena uwanjani kwenye mechi ya michuano ya Euro 2012, ambapo timu ya Hispania itakapocheza na Czech Republic na Scotland, mnamo tarehe 7 na 11 Oktoba.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ameweza kucheza jumla ya mechi 6 kwa klabu msimu huu, huku akikamilisha wastani wa dakika 469 uwanjani.

Bradley aajiriwa Misri



Inaarifiwa kwamba, Kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Marekani Bob Bradley, ameajiliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Misri.

Msemaji wa EFA Azmy Megahed amesema, Bradley anategemea kuwasili Cairo wikiendi hii kukamilisha mpango huo.

"Kila kitu kipo sawa. Bradley atawasili hapa siku ya Jumapili kukamilisha mkataba," Megahed alisema.

Bradley atakuwa amechukua nafasi ya kocha wa kipindi kirefu wa timu hiyo Hassan Shehata, ambaye kibarua chake kilisitishwa mnamo mwezi June, kufuatia kufanya vibaya kwa timu hiyo kwenye kampeni zake za kushiki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mwaka 2012.

Timu hiyo mpaka sasa imetolewa kwenye mbio hizo.

Bradley aliiwezesha Marekani kufika kwenye mzunguko wa 16 wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010, iliyofanyika nchini Afrika ya Kusini.

Na alipigwa chini mnamo mwezi July baada ya Marekani kufungwa 4-2 na Mexico kwenye fainali ya Gold Cup, huku nafasi yake ikichukuliwa na kocha wa zamani wa Ujerumani Jurgen Klinsmann.

Bradley atakuwa na mtihani mzito kuhakikisha nchi ya Misri inapata nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia, kwa mara ya mwisho Taifa hilo kushiriki Kombe hilo ilikuwa ni mwaka 1990.

Simba na Polisi zaingiza ml16/-


Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Polisi Dodoma iliyochezwa Septemba 14 mwaka huu Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 16,839,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 2,257 ambapo kiingilio kilikuwa sh, 7,000 kwa mzunguko na sh. 20,000 kwa VIP. Waliokata tiketi za sh. 20,000 walikuwa 80.

Baada ya kuondoa gharama za mchezo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 2,568,661.02 kila timu ilipata sh. 3,546,671.90. Mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja (sh. 1,162,893.90), TFF (sh. 1,162,893.90), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 581,446.95), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 465,157.56) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 116,289.39).

Kamati ya Tibaigana Sept. 24


Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakutana tena Septemba 24 mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza mashauri matatu dhidi ya Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage na Ofisa Habari wa klabu ya Yanga, Louis Sendeu.

Awali kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alfred Tibaigana ilikuwa ikutane Agosti 29 mwaka huu kusikiliza malalamiko ya TFF dhidi ya viongozi hao, lakini kikao kiliahirishwa kutokana na Kamati kutotimiza akidi (column) kwa wajumbe wake.

Pia TFF imewasilisha kwa kamati hiyo shauri jipya dhidi ya Sendeu kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi aliyechezesha mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Sendeu alimshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao, na anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba na kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima haikuwa halali.