Sergio Aguero anaonekana kuwa mchezaji muhimu ndani ya Manchester City, umuhimu kama aliokuwa nao Diego Maradona wakati alipokuwa anaichezea Napoli.
Aguero, ambaye amemuoa mtoto wa Maradona, amefunga magoli sita kwenye mechi nne alizoichezea City, toka ajiunge nayo kwa dau la £38 ml alipotokea timu ya Atletico Madrid, kwenye kipindi cha majira ya joto.
Na anapewa nafasi kubwa ya kuiongoza na kuiwezesha City kwenye ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza, kama ambavyo Maradona alifanya akiwa na Napoli.
Maradona aliiwezesha timu hiyo ya Italia kushinda Serie A mara mbili, Kombe la UEFA na Coppa Italia, wakati mchezaji huyo toka Argentina alipokuwa kwenye hiyo timu.
"Naamini ntaweza kuisaidia Manchester City kufanya mambo makubwa kama Diego alivyofanya akiwa na Napoli," Aguero alisema.
"Nimekuja hapa kuisaidia timu kukua na iweze kushinda makombe, na kama tukifanya hivyo mwaka huu itakuwa ni vizuri sana,. Ila tutajitahidi kuwa wazuri zaidi na nategemea kutoa mchango mkubwa kwenye hilo."