Thursday, September 15, 2011

Iniesta nje Mwezi Mmoja


Klabu ya Barcelona imetangaza kwenye mtandao wake kwamba, Andres Iniesta atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja.

Kiungo huyo aliumia dakika 5 kabla ya mapumziko, kwenye mechi ambayo timu yake ilitoka sare ya 2-2 na AC Milan, katika michuano ya Kombe la mabingwa Barani Ulaya siku ya Jumanne.

Iniesta atakosa mechi dhidi ya Osasuna, Valencia, Atletico Madrid, BATE Borisov na Sporting Gijon.

Mchezaji huyo anategemea kurudi tena uwanjani kwenye mechi ya michuano ya Euro 2012, ambapo timu ya Hispania itakapocheza na Czech Republic na Scotland, mnamo tarehe 7 na 11 Oktoba.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ameweza kucheza jumla ya mechi 6 kwa klabu msimu huu, huku akikamilisha wastani wa dakika 469 uwanjani.

Bradley aajiriwa Misri



Inaarifiwa kwamba, Kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Marekani Bob Bradley, ameajiliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Misri.

Msemaji wa EFA Azmy Megahed amesema, Bradley anategemea kuwasili Cairo wikiendi hii kukamilisha mpango huo.

"Kila kitu kipo sawa. Bradley atawasili hapa siku ya Jumapili kukamilisha mkataba," Megahed alisema.

Bradley atakuwa amechukua nafasi ya kocha wa kipindi kirefu wa timu hiyo Hassan Shehata, ambaye kibarua chake kilisitishwa mnamo mwezi June, kufuatia kufanya vibaya kwa timu hiyo kwenye kampeni zake za kushiki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mwaka 2012.

Timu hiyo mpaka sasa imetolewa kwenye mbio hizo.

Bradley aliiwezesha Marekani kufika kwenye mzunguko wa 16 wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010, iliyofanyika nchini Afrika ya Kusini.

Na alipigwa chini mnamo mwezi July baada ya Marekani kufungwa 4-2 na Mexico kwenye fainali ya Gold Cup, huku nafasi yake ikichukuliwa na kocha wa zamani wa Ujerumani Jurgen Klinsmann.

Bradley atakuwa na mtihani mzito kuhakikisha nchi ya Misri inapata nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia, kwa mara ya mwisho Taifa hilo kushiriki Kombe hilo ilikuwa ni mwaka 1990.

Simba na Polisi zaingiza ml16/-


Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Polisi Dodoma iliyochezwa Septemba 14 mwaka huu Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 16,839,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 2,257 ambapo kiingilio kilikuwa sh, 7,000 kwa mzunguko na sh. 20,000 kwa VIP. Waliokata tiketi za sh. 20,000 walikuwa 80.

Baada ya kuondoa gharama za mchezo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 2,568,661.02 kila timu ilipata sh. 3,546,671.90. Mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja (sh. 1,162,893.90), TFF (sh. 1,162,893.90), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 581,446.95), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 465,157.56) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 116,289.39).

Kamati ya Tibaigana Sept. 24


Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itakutana tena Septemba 24 mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza mashauri matatu dhidi ya Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage na Ofisa Habari wa klabu ya Yanga, Louis Sendeu.

Awali kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alfred Tibaigana ilikuwa ikutane Agosti 29 mwaka huu kusikiliza malalamiko ya TFF dhidi ya viongozi hao, lakini kikao kiliahirishwa kutokana na Kamati kutotimiza akidi (column) kwa wajumbe wake.

Pia TFF imewasilisha kwa kamati hiyo shauri jipya dhidi ya Sendeu kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi aliyechezesha mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Sendeu alimshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao, na anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba na kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima haikuwa halali.

Wednesday, September 14, 2011

Fergie: Rooney ni kama Pele


Meneja wa klabu ya Manchester United Sir Alex Ferguson, amemfananisha mshambuliaji wa timu yake Wayne Rooney na mchezaji mkongwe wa Brazil Pele.

Fergie ameyasema hayo, kuelelekea kwenye mechi ya Kombe la Klabu Bingwa ya Ulaya dhidi ya Benfica, mechi inayotarajiwa kuchezwa usiku huu, huku mchezaji huyo akionekana kuwa kwenye kiwango kizuri kiuchezaji.

Tuesday, September 13, 2011

Upatikanaji wa Tiketi mechi za Simba na Yanga Uwanja wa Chamazi


Tiketi kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zinazohusisha timu za Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam hazitauzwa uwanjani. Lengo ni kuwaondolea usumbufu mashabiki ambao wanakwenda kwenye mechi hizo na kukuta tiketi zimekwisha, hivyo kuweza kuwa chanzo cha vurugu.

Ili kujiridhisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilifanya uhakiki na kubaini Uwanja wa Azam una uwezo wa kuchukua watazamaji 5,000 tu na si 7,000 kama ilivyoelezwa awali. Hata hivyo lengo la mmiliki wa uwanja huo ni kuongeza viti hadi kufikia 7,500.

Kwa mantiki hiyo tiketi zitakazouzwa kwa mechi za Yanga na Simba kwenye uwanja huo ni 5,000 tu. Vituo vya kuuzia tiketi hizo siku moja kabla ya mchezo na siku yenyewe ya mchezo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha Mafuta cha OilCom kilichoko Ubungo na Mbagala Rangitatu.

Viingilio kwa mechi za timu hizo zitakazochezwa Uwanja wa Azam ni sh. 20,000 kwa jukwaa kuu lenye uwezo wa kuchukua watazamaji 400 wakati majukwaa ya kawaida itakuwa sh. 7,000. Ili kuhakikisha idadi ya mashabiki haizidi uwezo wa uwanja hakutakuwa na tiketi za bure (complimentary).

Hivyo kutokana na kuwepo vituo vya kuuzia tiketi katika maeneo yaliyotajwa, mashabiki ambao watakosa tiketi hawana sababu ya kwenda uwanjani. Simba na Yanga zitaanza kuutumia uwanja huo kesho (Septemba 14 mwaka huu) kwa Simba kuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma wakati siku inayofuata Yanga itakuwa mgeni wa African Lyon.

Sendeu kwa Pilato Tibaigana



Sekretarieti ya TFF itawasilisha mashtaka dhidi ya Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu kwenye Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi inayoongozwa na Kamishna wa Polisi mstaafu Alfred Tibaigana kutokana na matamshi yake dhidi ya mwamuzi Alex Mahagi.

Mara baada ya mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Sendeu aliita mkutano na waandishi wa habari na kumshutumu Mahagi kuwa alisababisha timu yake ikose ushindi kwa kuwabeba wapinzani wao.

Aliongeza kuwa anamfahamu Mahagi kuwa ni mwanachama wa Simba, kadi nyekundu aliyompa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima si halali na alifanya hivyo kwa lengo la kuisadia Simba ili iendelee kukaa kileleni mwa ligi.

Kauli ya Sendeu ililenga kumjengea chuki Mahagi mbele ya mashabiki wa Yanga kama ilivyo kwa viongozi na watendaji wa TFF. Ni wazi Sendeu akiwa ofisa wa Yanga anajua taratibu za kufanya pale klabu yake isiporidhishwa na uamuzi wa mwamuzi au suala lingine lolote.

Matamshi ya Sendeu yanalenga kuchochea chuki na vurugu katika mpira wa miguu ambapo ni kinyume na Ibara ya 53(1) na (2) ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Kombe la Mabingwa Barani Ulaya

Usikose uhondo huu kuanzia Saa 3:45 Usiku

Bayern Munich | Villarreal | Manchester City | Napoli
Inter Milan | CSKA Moscow | Lille | Trabzonspor
Manchester United | Benfica | Basel | Otelul Galati
Real Madrid | Lyon | Ajax | Dinamo Zagreb
Chelsea| Valencia | Bayer Leverkusen | Genk
Arsenal | Marseille | Olympiakos | Borussia Dortmund
FC Porto | Shakhtar Donetsk | Zenit St Petersburg | APOEL
Barcelona | AC Milan | BATE Borisov | Viktoria Plzen

Mechi za CL

Jumatano Sept. 14
Ajax v Lyon, GpD, 21:45
Basle v SC Otelul Galati, GpC, 21:45
Benfica v Man Utd, GpC, 21:45
Dinamo Zagreb v Real Madrid, GpD, 21:45
Inter Milan v Trabzonspor, GpB, 21:45
Lille v CSKA Moscow, GpB, 21:45
Man City v Napoli, GpA, 21:45
Villarreal v Bayern Munich, GpA, 21:45

Saa 3:45 Usiku

Muda ni kwa saa za Bongo

Barca yashikwa shati saa ya kifo

 
AC Milan wameweza kupata sare ya bao 2-2 dhidi ya Barcelona, baada ya mpira wa kichwa uliopigwa na Thiago Silva kutinga wavuni, kufuatia kona iliyopigwa na mkongwe Seedorf kwenye dakika za nyongeza za mechi kuisha.
 
Alex Pato aliushangaza umati wa washabiki wa Camp Nou, baada ya kuifunga moja ya goli la kihistoria ya michuano hiyo, mchezaji huyowa kimataifa toka Brazil, lifunga goli kwenye sekunde ya 24 mara tu baada ya mpira kuanza, na kuwafanya Milan wawe mbele kwa bao moja.
 
Barca walipigana kiume, ambapo Pedro aliweza sawazisha goli kwa shuti la karibu, halafu David Villa akaongeza la pili kutokana na mpira wa adhabu.
 
Arsenal waliporwa tonge mdomoni, baada ya bao la Ivan Perisic alilolifunga dakika za majeruhi kuiwezesha Dortmund kupata sare ya goli 1-1, huku goli la Arsenal likiwekwa kimiani na Robie Van Persie.
 
Kwengineko Porto, Chelsea, Apoel Nicosia na Marseille walianza vyema michuano hiyo kwa ushindi.
 
Matokeo ya Mechi za CL
Jumanne, 13 September 2011
 
Apoel Nicosia 2-1 Zenit St Petersburg
Barcelona 2-2 AC Milan
Borussia Dortmund 1-1 Arsenal
Chelsea 2-0 Bayer Leverkusen
FC Porto 2-1 Shakhtar Donetsk
Genk 0-0 Valencia
Olympiakos 0-1 Marseille
Plzen 1-1 BATE Borisov

Ibrahimovic kukosa mechi ya Barcelona


 
Mshambuliaji wa timu ya AC Milan Zlatan Ibrahimovic, ameondolewa kwenye kikosi cha timu hiyo, na hivyo atakosa kukutana na timu yake ya zamani Barcelona.
Mechi hii ya kwanza ya Michuano ya Kombe la Mabingwa Bara la Ulaya Kundi H, itachezwa leo kwenye Uwanja wa Camp Nou.
Ibrahimovic alipata maumivu kwenye mguu, wakati wa mazoezi ya timu hiyo siku ya Jumatatu, maumivu yaliyosababisha kuachwa kwenye msafara huo ulioelekea Hispania.

Kombe la Mabingwa Barani Ulaya

Usikose uhondo huu kuanzia Saa 3:45 Usiku

 
Group A
Bayern Munich | Villarreal | Manchester City | Napoli
Group B
Inter Milan | CSKA Moscow | Lille | Trabzonspor
Group C
Manchester United | Benfica | Basel | Otelul Galati
Group D
Real Madrid | Lyon | Ajax | Dinamo Zagreb
Group E
Chelsea| Valencia | Bayer Leverkusen | Genk
Group F
Arsenal | Marseille | Olympiakos | Borussia Dortmund
Group G
FC Porto | Shakhtar Donetsk | Zenit St Petersburg | APOEL
Group H
Barcelona | AC Milan | BATE Borisov | Viktoria Plzen


Mechi za LEO:

Apoel Nicosia v Zenit St Petersburg, GpG, 21:45
Barcelona v AC Milan, GpH, 21:45
Borussia Dortmund v Arsenal, GpF,21:45
Chelsea v Bayer Leverkusen, GpE, 21:45
FC Porto v Shakhtar Donetsk, GpG, 21:45
Genk v Valencia, GpE, 21:45
Olympiakos v Marseille, GpF, 21:45
Plzen v BATE Borisov, GpH, 21:45 
Muda ni kwa saa za Bongo, Saa 3:45 Usiku

Ferdinand aachwa safari ya Ureno

Beki wa Timu ya Man U Rio Ferdinand, hajasafiri na Timu hiyo nchini Ureno kwenye mechi ya Ufunguzi Kombe la Mabigwa Barani Ulaya, mchezo utakaochezwa siku ya Jumatano dhidi ya Benfica.
Hajaelewaka moja kwa moja nini hasa sababu iliyofanya kuachwa kwake, ila inaaminika ni katika kumpa mapumziko zaidi mchezaji huyo.
Toka msimu mpya uanze mechi ya juzi dhidi ya Bolton ndio ilikuwa mechi yake ya kwanza kucheza kwa dakika zote 90 za mchezo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, sambamba na Nemanja Vidic ambaye mara kwa mara huwa wanacheza nafasi ya ulinzi wa kati wa timu hiyo naye pia hatokuwepo kwenye kikosi hicho.
Jonny Evans anategemea kuungana na beki mgeni wa kikosi hicho Phil Jones kuziba mapengo hayo.

Monday, September 12, 2011

Aguero: Ajipanga kuwa Maradona wa City


Sergio Aguero anaonekana kuwa mchezaji muhimu ndani ya Manchester City, umuhimu kama aliokuwa nao Diego Maradona wakati alipokuwa anaichezea Napoli.

Aguero, ambaye amemuoa mtoto wa Maradona, amefunga magoli sita kwenye mechi nne alizoichezea City, toka ajiunge nayo kwa dau la £38 ml alipotokea timu ya Atletico Madrid, kwenye kipindi cha majira ya joto.

Na anapewa nafasi kubwa ya kuiongoza na kuiwezesha City kwenye ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza, kama ambavyo Maradona alifanya akiwa na Napoli.

Maradona aliiwezesha timu hiyo ya Italia kushinda Serie A mara mbili, Kombe la UEFA na Coppa Italia, wakati mchezaji huyo toka Argentina alipokuwa kwenye hiyo timu.

"Naamini ntaweza kuisaidia Manchester City kufanya mambo makubwa kama Diego alivyofanya akiwa na Napoli," Aguero alisema.

"Nimekuja hapa kuisaidia timu kukua na iweze kushinda makombe, na kama tukifanya hivyo mwaka huu itakuwa ni vizuri sana,. Ila tutajitahidi kuwa wazuri zaidi na nategemea kutoa mchango mkubwa  kwenye hilo."

Evra: Lazma tuwe makini

  
Patrice Evra amewaasa wachezaji wenzake wa Manchester United, kuwa makini na kuendelea kukaza buti baada ya kuanza msimu mpya wa ligi kwa rekodi nzuri.

"Tunafanya na inaonekana kama rahisi, lakini si kweli." Alisema alipokuwa anaongea na gazeti la The Independent, "Ninawaheshimu sana Manchester City - wana kikosi makini sana."

"Walipoifunga Tottenham 5-1, tuliiangalia mechi na tukasema ni vyema tukacheza vizuri tukikutana na Arsenal - na tukafanikiwa kushinda kwa goli nane."

"Inaonekana kama ni mashindano kati ya timu hizi mbili, ila msisahaua Chelsea na Liverpool. Japokuwa, kila niwaonapo watu kitu cha kwanza kwao kuuliza ni tarehe ya mechi na wapinzani wetu."

Viingilio Mechi za Chamazi

Timu za Simba na Yanga zitaanza kuutumia Uwanja wa Azam Chamazi ulioko Mbande, Dar es Salaam wiki hii. Septemba 14 mwaka huu Simba itakuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma wakati siku inayofuata African Lyon itakuwa mwenyeji wa Yanga.

Kwa mujibu wa msemaji wa Shirikisho hili Boniface Wambura, Viingilio kwa mechi zinazohusisha timu za Yanga na Simba kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 7,000 tu vitakuwa sh. 15,000 kwa jukwaa kuu na sh. 5,000 mzunguko.

Kwa timu nyingine za Dar es Salaam zinazotumia uwanja huo kiingilio kitaendelea kuwa kile kile cha sh. 10,000 jukwaa kuu na sh. 3,000 mzunguko.

Simba na Azam zaingiza Ml. 72


Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Azam na Simba iliyochezwa Septemba 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 72,167,000.

Kwa mujibu wa msemaji wa Shirikisho hili Boniface Wambura, Watazamaji waliokata tiketi kwa ajili ya kushuhudia mechi hiyo walikuwa 21,129. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 15,000, sh. 7,000, sh. 5,000 na sh. 3,000.

Viti vya bluu na kijani ambavyo kiingilio kilikuwa sh. 3,000 viliingiza watazamaji 18,586, hivyo kuingiza sh. 55,758,000.

Marekebisho Mechi za Uwanja wa Taifa

Ili kutekeleza maagizo ya Serikali kucheza mechi mbili tu za Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa, Shirikisho la Soka Nchini (TFF) limefanya marekebisho kwa baadhi ya mechi zilizokuwa zichezwe kwenye uwanja huo.

Kwa mujibu wa msemaji wa Shirikisho hili Boniface Wambura sasa, mechi zitakazochezwa Uwanja wa Taifa ni – mechi namba 39- Azam vs Yanga (Septemba 18), mechi namba 50- Simba vs Mtibwa Sugar (Septemba 25), mechi namba 52- Yanga vs Coastal Union (Septemba 28) na mechi namba 58- Yanga vs Kagera Sugar (Oktoba 13).

Nyingine ni mechi namba 62- Simba vs African Lyon (Oktoba 16), mechi namba 65- Yanga vs Toto Africans (Oktoba 20), mechi namba 72- Simba vs JKT Ruvu (Oktoba 22), mechi namba 78- Yanga vs Simba (Oktoba 29) na mechi namba 86- Moro United vs Simba (Novemba 2).

Mechi zifuatazo zitachezwa Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam; mechi namba 35- Simba vs Polisi Dodoma (Septemba 14), mechi namba 29- African Lyon v Yanga (Septemba 15), mechi namba 45- Yanga vs Villa Squad (Septemba 21), mechi namba 66- Simba vs Ruvu Shooting (Oktoba 19) na mechi namba 71- Yanga vs Oljoro JKT (Oktoba 23).

Mapato Mechi ya Yanga na Ruvu Shooting


Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa Septemba 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 23,388,000.

Kwa mujubu wa taarifa iliyotumwa kwa Yyombo vya Habari na Ofisa Habari na Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Boniface Wambura, inasema  Watazamaji waliokata tiketi kwa ajili ya kushuhudia mechi hiyo walikuwa 6,566. Viingilio vilikuwa sh. 15,000, sh. 7,000, sh. 5,000 na sh. 3,000.

Sunday, September 11, 2011

Salha Israel: Miss TZ 2011


Hatimaye zoezi lililochukua miezi kadhaa la kumtafuta mrembo mpya wa Tanzania kwa mwaka huu wa 2011(Miss Tanzania 2011), lilifikia kilele chake jana usiku katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar-es-salaam na mwanadada Salha Israel kuibuka mshindi na hivyo kuvikwa rasmi taji la Miss Tanzania 2011 kutoka kwa Genevive Emmanuel Mpangala (Miss Tanzania 2010) aliyekuwa akilishikilia taji hilo mpaka hapo jana.

Katika kilele cha shindano hilo lililodhaminiwa kwa kiasi kikubwa na kampuni ya Vodacom na kupambwa na burudani ya mziki kutoka kwa wasanii mbalimbali wanaotamba Afrika Mashariki na Kati kama vile Diamond,Bob Junior,Kidumu na wengineo,mshindi wa pili alikuwa Tracy Sospeter na mshindi wa tatu akawa Alexia William.

Saturday, September 10, 2011

Mrithi wa Genevive kupatikana leo

Genevive Miss Tanzania 2010
SHINDANO la kumsaka mrembo wa Miss Tanzania linafanyika leo kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Jumla ya warembo 30 watapanda jukwaani kuchuana vikali kuwania zawadi ya gari aina ya Jeep Patriot yenye thamani ya shilingi 72 milioni.
Warembo hao wataonyesha vazi la ubunifu, ufukweni na vazi la usiku.
Mshindi atapata fursa ya kuiwakilisha Tanzania kwenye shindano la urembo la dunia 'Miss World' litakalofanyika baadaye mwaka huu.

Yanga kukata kiu ya mashabiki wake leo?

Mashabiki wa Yanga
MASHABIKI wa Yanga wenye kiu ya ushindi wa takribani siku 62, watajazana kwenye Uwanja Taifa kuwaongoza mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu kusaka pointi tatu dhidi ya vibonde Ruvu Shooting leo.

Yanga wanashuka uwanjani hapo wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba katika mechi ya fainali ya Kombe la Kagame iliyofanyika Julai 10 yakiwa ni matokeo yao mazuri ya mwisho katika mechi zaidi ya saba walizocheza tangu wacheze mechi hiyo.

Mabingwa hao walikuwa kwenye wakati mgumu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro waliouteua kuwa uwanja wa nyumbani baada ya serikali kuufunga Uwanja wa Taifa kwa takribani wiki mbili.

Katika mchezo wa leo dhidi ya Shooting, vijana hao wa mtaa wa Twiga na Jangwani wanajua mashabiki wao wana hamu kubwa ya kuona timu hiyo ikirudisha heshima yake kwa kushinda mchezo wa kwanza katika Ligi Kuu.

Picha Bora ya Wiki ya Kimichezo

Luis Suarez

Maradona: Sijawahi angalia mechi ya Argentina

Diego Maradona

Kocha wa timu ya Al-Wasl Diego Maradona, amesema hawezi thubutu kuangalia mechi ya Timu ya Taifa ya Argentina.
Kocha huyo ambaye hivi karibuni ameanza kutafuta mafanikio mapya Mashariki ya Kati amesema, " Toka nilipoondoka, sijawahi kuangalia hata mechi moja ya Argentina"
"Sidhani kama ntakuja kuangalia tena, najua itaniumiza" alisema nguli huyo wa zamani mwenye miaka 50 sasa.

"Sina deni na mtu, nilijitahidi kujitoa kwa yote kwa wachezaji, nao walifanya kwangu kama mimi ilivyofanya kwao."

"Hatukuweza kuwapa Wa-Argentina kile walichopaswa kukipata, ambacho kilikuwa ni Kombe la Dunia, ila tulijitahidi kadiri tulivyoweza, na tunajiangalia kwenye kioo na fahari."
Zlatan Ibrahimovic

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Italia maarufu kama Seria A AC Milan, wameshindwa kuanza vyema kutetea taji hilo, baada ya kwenda sare ya 2-2 na Lazio, kwenye uwanja wao wa San Siro jana Ijumaa.
Wageni ndio waliokuwa wa kwanza kuingiza nyavuni bao zote mbili, kwa magoli yaliyofungwa na washambuliaji wapya Miroslav Klose na Djibril Cisse.
Zlatan Ibrahimovic na Antonio Cassano waliweza kuipatia Inter magoli ya kusawazisha na kuifanya mechi iishe kwa sare.

Mechi za EPL leo Jumamosi

Jumamosi, 10 September 2011
Muda ni kwa Saa za Bongo


Arsenal v Swansea, 17:00
Everton v Aston Villa, 17:00
Man City v Wigan, 17:00
Stoke v Liverpool, 17:00
Sunderland v Chelsea, 17:00
Wolverhampton v Tottenham, 17:00
Bolton v Man Utd, 19:30

Tevez anyang'anywa Unahodha City

Carlos Tevez

Carlos Tevez amenyang'anywa rasmi Unahodha wa timu ya Man City na Meneja wa Timu hiyo Roberto Mancini.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentine, ambaye kwa kipindi kirefu cha usajili amekuwa akitafuta timu ya kuhamia, nafasi yake ya Unahodha amepewa mlinzi wa timu hiyo Vincent Kompany.
Mancini alisema: "Carlos alikuwa anataka kuondoka kwa sababu za kifamilia, nikaheshimu maamuzi yake, ila Carlos bado yuko hapa sababu hatukupata ufumbuzi.
"Niliamua kwenye kipindi cha majira ya joto Vinnie [Kompany] ndiye awe Nahodha wa timu."

Young: Hakuna uhakika wa namba United

Ashley Young

Licha ya kuanza vyema msimu kama mchezaji wa Manchester United, Ashley Young anasema inabidi aendelee kukaza buti ili aweze kuendelea kuwemo kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Mchezaji huyo wa kimataifa toka Uigereza amejiunga na Mashetani Wekundu kwa gharama ya £15 ml toka Klabu ya Aston Villa katika kipindi cha majira ya joto, huku akiweza kuendana haraka na mfumo wa kimchezo wa vijana wa Old Trafford.
Ameweza kufunga magoli mawili kwenye mechi ya Pemier League dhidi ya Arsenal, mechi iliyoisha kwa Man U kupata ushindi wa goli 8-2, huku akitoa pasi nne za kufunga.
Uwepo wa Ryan Giggs, Park Ji-Sung na Antonio Valencia ni ishara tosha ya ugumu wa namba kwenye nafasi yake.
"Mazingira kwenye nafasi yangu ni mazuri, najisikia kama nimepokewa kwa mikono miwili," Young alisema. "Nimeweza kuendana na mfumo wa kikosi haraka, binasfi naona ni rahisi kuendana nao."
"Kila mtu ana hali ya ushindi na anataka namba kwenye kikosi cha kwanza - inabidi kuwa makini."

Thursday, September 8, 2011

Maria Mutola ajiunga na Soka

Maria Mutola


Wakati Maria Mutola alipomaliza fainali za mbio mita 800 kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Beijing, huku akiwa na umri wa miaka 35, ilionekana kwamba huo ndio ungekuwa mwisho wa mwana mama huyo aliyepachikwa jina la "Maputo Express" kwenye dunia ya kimichezo.

Ila baada ya miaka mitatu, akiwa amestaafu kwenye mbio, Mutola ameamua kujikita kwenye mpira wa miguu, na safari hii akiwa nahodha wa timu ya Msumbiji

Mutola, anaiwakilisha nchi hiyo kwenye mashindano ya All-Africa Games yanayoendelea nchini kwao kwenye jiji la Maputo. 

Mertesacker ajifananisha na Tonny Adams

Per Mertesacker

Beki mpya wa Arsenal Mjerumani Per Mertesacker, anaamini ataweza kufata nyayo za beki wazamani wa timu hiyo Tony Adams, hii ni katika kuelekea kwenye mechi yake ya kwanza akiwa na washika bunduki wa Emirate siku ya Jumamosi dhidi ya Swansea.

Mertesacker anatakiwa aendane na mfumo wa vijana wa Wenger haraka, beki wa timu hiyo Thomas Vermaelen yuko atakuwa nje ya dimba kwa wiki sita, baada a kufanyiwa upasuaji wa enka siku ya Jumatatu.
Mjerumani huyo, ambaye amejiunga na Klabu hiyo akitokea Werder Bremen kwa gharama ya £8 ml, anataka kuwa sehemu ya wachezaji watakao rudisha mafanikio ya timu ya Arsenal.
Tonny Adam alikuwa nahodha wa timu hiyo kwenye moja kati ya vipindi vya mafanikio ya Klabu hiyo, Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal aliiwezesha timu hiyo kushinda vikombe Vinne vya Ligi, huku wakati flani akiweza kubeba kombe hilo mara mbili mfululizo chini ya Wenger.
"Hatukuwa na taswira yake kwenye Tv, ila Adam aliheshimika sana hapa, yeye ni mtu muhimu kwangu," Mertesacker aliueleza mtandao wa Klabu ya hiyo. 

"Nilipokuwa naangalia Ligi ya Uingereza, mara nyingi nilikuwa nawaatazama Arsenal, hakika alikuwa ni beki mzuri sana, kipindi hicho nikiwa na miaka 10 au 12 hivi, nawapenda wachezaji kama  Adams sana tu – Nimekuwa nikifurahi kuwangalia kwa miaka mingi.
" Natumai nitaongeza kiwango changu hapa na kuwa bora na bora – nataka niwe mtu muhimu kwenye timu."

Ronaldo: Nataka kushinda CL na Madrid

Cristiano Ronaldo

Mshambuliaji wa timu ya Real Madrid Cristiano Ronaldo, amesema shabaha yake kuu msimu huu ni kushinda Champions League.
Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United, anaamini kushinda Kombe hilo la Ulaya ndio yatakuwa mafanikio makubwa pale Santiago Bernabeu kwa msimu huu.
"Inatubidi tushinde Makombe muhimu, La Liga au Champions League sababu, haya ndiyo makombe yanayokufanya uone kama umeshinda kitu kwenye mpira," aliueleza mtandao wa Uefa.
"Kushinda Champions League ni hatua ya mwisho kuhesabu kwamba umemaliza msimu sababu ni moja kati ya makombe muhimu.
Madrid watakutana na Dinamo Zagreb wiki ijayo kwenye Champions League, ikiwa ni mchezo wa kwanza wa Kundi D, kabla ya hapo wataanza kuwakaribisha Getafe kwenye uwanja wa nyumbani Santiago Bernabeu, katika mechi ya La Liga siku ya Saturday.

Usishangae Beckham QPL January

David Beckham

Litakapokuja kufunguliwa dirisha la usajili, usishangae Queens Park Rangers wakionyesha nia ya kumtaka David Beckham, ambaye mkataba wake kwenye Major League Soccer unaisha mwezi November.
"Ila hiyo haitakuwa mpaka mwezi January, hakika hiki si kitu cha kuzungumza kwa sasa." Haya ni maneno ya Kocha mkuu wa timu hiyo Neil Warnock.
"Hatuwezi kumsajili ila, hatuwezi kumsajili mtu yoyote kwa sasa mpaka January, kwa nini muwe na wasi?" Warnock alisema siku ya Alhamisi, wiki moja baada ya dirisha la usajili kufungwa.
"Nadhani ni mchezaji wa kipekee, na amekuwa hazina kubwa kwa soka la Uingereza, nampenda kama mtu ila niulize itapofika January.” Alisema Warnock.

Guardiola apewa tunzo na Bunge la Catalonia

Pep Guardiola

Kocha wa Klabu ya Barcelona Pep Guardiola, amepewa Tunzo ya Dhahabu ya mafanikio na Bunge la Catalonia.

Tunzo hiyo inatambua mchango wake toka alipoichukua timu hiyo kipindi cha majira ya joto ya mwaka 2008, baada ya kuwa kocha wa timu B ya Barcelona kwa mwaka mmoja.

"Nilichaguliwa kuwa Kocha wa Barca na faida ilikuwa ni kwa wale walionichagua, huku hii ikiwa njia nzuri ya kukabiliana na kazi yangu," alisema.

Guardiola ameiongoza na kuipa Barca jumla ya makombe 12, mawili ya Kombe la Mabingwa Ulaya, na matatu yakiwa ni mataji ya La Liga.

Balotelli ahusishwa na Kundi la Kijasusi la Mafia

Mario Balotelli
Mikasa inayomkumba Mario Balotelli toka ajiunge na Klabu ya Manchester City imechukua hatua nyingine, safari hii mchezaji anatakiwa na Jeshi la Polisi la nchini Italia kuelezea mahusiano yake na Kundi la Kijasusi la Mafia.

Balotelli, ambaye amejiunga na Klabu hiyo kwa wa £24 ml toka Inter Milan mnamo mwaka jana, ameitwa kama shahidi na waendesha mashtaka wa jiji la Naples, lengo likiwa ni kuweza kusaidia uchunguzi unaoikabili kundi la Mafia.
Inasemekana mchezaji huyo, alionekana akiwa sambamba kwenye msafara wa moja kati ya makundi ya kiharifu yaliyopo jijini Naples, makundi yanayoongozwa na Mario Iorio, mmoja kati ya watu wanaojishughulisha na biashara ya kusambaza vyakula.
Huku ikielezwa, Lorio anahusishwa na kashfa ya utengenezaji noti bandia, kesi yake ikiwa inaendelea.

"Hakuna kitu cha kuogopa, niko poa, sikuwa na wazo na watu waliokuwa wanapita karibu yangu ni kina nani," Balotelli alisema alipoulizwa kuhusiana na ishu hiyo.
"Siku ile kulikuwa na watu wengi karibu yangu, najisikia vibaya sababu inaweza kuithiri familia yangu, nilichokuwa nataka nione pale ni namna gani lile eneo linafanana na vile ambavyo huwa naliona kwenye filamu ya Gomorrah."

Rooney amuhitaji Chicharito haraka

Rooney & Hernandez

Wayne Rooney amesema, angependa kuungana na mchezaji mwenzake Javier Hernandez kwenye safu ya ushambulizi ya timu hiyo mapema zaidi.

Wachezaji hao wawili, msimu uliopita wa EPL walitengeneza safu kali ya ushambuliaji, safu iliyosaidia kuipa Manchester United ubingwa wake wa 19 wa Ligi hiyo.

"Naamini tulichokifanya na Hernandez msimu uliopita tutakifanya pia msimu huu, tutafunga magoli mengi," Rooney aliieleza MUTV.

"Hakika watu wanamfahamu kwa sasa ila, kama ukiangalia wachezaji wakali Duniani, huwa wanafahamu wanacheza na nani na ni ngumu kuwazuia.

"Mienendo yake ndani ya uwanja ni mizuri, na ni ngumu kuizuia. Si rahisi kwa wachezaji kumzuia, wawe wanamfahamua ama kinyume chake.

"Ni vizuri kuwa na mwenza ambaye amefika kwenye timu, ambaye anaweza kuongea Kingereza kizuri na kila wakati ana tabasamu." Alisema Rooney.

Ayew kukosa mechi ya ufunguzi CL

Andre Ayew

Mchezaji nyota wa Timu ya Taifa ya Ghana Andre Ayew, atakosa mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, wakati timu yake ya Marseille itakapokuwa inacheza na Olympiakos siku ya Jumanne.

Ayew 21, anasumbuliwa na maumivu ya kifundo, yatamsababisha pia asiwepo kwenye mechi ya kwanza ya Ligue 1, ambayo Timu yake itacheza dhidi ya Stade Rennes wekiendi hii.

"Andre Ayew anategemea kuwa nje ya uwanja kwa siku 10, baada ya kuumia kwenye mechi aliyokuwa anaitumikia Ghana," FA ya Ghana imeeleza kwenye mtandao wake leo.

"Mchezaji huyo wa Marseille alipata jeraha hilo wakati Ghana ilipokuwa inacheza na Swaziland, kwenye mechi ya kusaka nafasi ya kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika Ijumaa iliyopita." Taarifa hiyo ilisema.

Twiga Stars yatoka sare na Banyana


Timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) imetoka sare ya mabao 2-2 na Afrika Kusini (Banyana Banyana) katika mechi ya michezo ya All Africa Games (AAG) iliyochezwa leo Uwanja wa Machava jijini Maputo, Msumbiji.

Banyana Banyana ndiyo iliyoanza kupata bao kabla ya Twiga Stars kusawazisha dakika ya 25 kupitia kwa Mwanahamisi Shuruwa.

Banyana Banyana ilianza kipindi cha pili kwa nguvu na kupata bao la pili. Zena Khamis aliisawazishia Twiga Stars dakika 60.

Twiga Stars itacheza mechi yake ya mwisho hatua ya makundi Septemba 11 mwaka huu dhidi ya Zimbabwe kwenye uwanja huo huo. Katika mechi yake ya kwanza Zimbabwe ilifungwa na Banyana Banyana mabao 4-1.

Tarehe ya Rufaa ya Bin Hammam yatajwa

Mohamed Bin Hammam

Shauri la aliyekuwa mgombea nafasi ya Urais wa FIFA Mohamed Bin Hammam, juu ya kupinga adhabu ya kifungo cha maisha aliyopewa kutojihusisha na masuala ya mpira, limepangwa kusikilizwa wiki ijayo.

FIFA wamethibitisha.

Kamati ya rufaa ya FIFA, inategemea kusikiliza shauri hilo siku ya Alhamisi, September 15, ambapo Bin Hammam anapinga adhabu hiyo, iliyotolewa na kamati ya maadili ya Shirikisho hilo mnamo mwezi July.

Shauri hilo linaweza kamilika siku hiyo japo kuna uwezekano linaweza kwenda mpaka September 16.

Simba na Yanga ruhsa kutumia Uwanja wa Taifa

Uwanja wa Taifa

Serikali imeruhusu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinazohusu timu za Simba na Yanga. Hata hivyo ruhusa hiyo ni ya mechi mbili kwa wiki.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu za VPL zenye maskani yake Dar es Salaam waliwasilisha tena maombi Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ili kutumia uwanja huo kwa mechi za ligi.

Kutokana na uamuzi huo wa Serikali mechi ambazo sasa zitachezwa kwenye uwanja huo ni Ruvu Shooting vs Yanga (Septemba 10), Azam vs Simba (Septemba 11), Simba vs Polisi Dodoma (Septemba 14), African Lyon v Yanga (Septemba 15), Azam vs Yanga (Septemba 18), Yanga vs Villa Squad (Septemba 21).

Nyingine ni Yanga vs Coastal Union (Septemba 24), Simba vs Mtibwa Sugar (Septemba 25), Yanga vs Kagera Sugar (Oktoba 14), Simba vs African Lyon (Oktoba 16), Simba vs Ruvu Shooting (Oktoba 19), Yanga vs Toto Africans (Oktoba 20), Simba vs JKT Ruvu (Oktoba 22), Yanga vs Oljoro (Oktoba 23), Yanga vs Simba (Oktoba 29) na Moro United vs Simba (Novemba 5).

Nafasi ya Torres Hispania shakani

Fernando Torres

Fernando Torres ameelezwa na Kocha wa Timu ya Taifa lake Vicente del Bosque kwamba, anaweza kupoteza nafasi yake kwenye kikosi hicho, kama atashindwa kufunga magoli mara kwa mara kwenye timu yake ya Chelsea .

Nafasi yake kwenye timu ya Chelsea inatishiwa na uwepo wa wachezaji kama Didier Drogba, Nicolas Anelka na Romelu Lukaku, kitu ambacho kinatisha nafasi yake pia kwenye timu ya taifa. lake.

Del Bosque hakumpa nafasi Torres hata yakuwepo kwenye benchi, kwenye mechi ambayo Hispania ilishinda kwa magoli 6-0 dhidi ya Liechtenstein, kitendo kilichomfanya mshambuliaji huyo kuangalia mechi hiyo akiwa jukwaaini.

"Torres ni mchezaji muhimu, ila wale wanaofanya vizuri kwenye klabu zao ndio wataoitwa timu ya Taifa, na si kinyume na hapo," alisema Del Bosque.

Torres hajaifungia timu yake ya taifa toka alipofunga kwenye mechi dhidi ya Liechtenstein miezi 12 iliyopita.

Dalglish amtetea Carroll

Andy Carroll

Meneja wa Klabu ya Liverpool Kenny Dalglish, amemtetea mchezaji wake Andy Carroll, kufuatia shutuma alizotupiwa na Kocha wa Timu ya Taifa ya Uingereza Fabio Capello, juu ya kiwango cha mchezaji huyo na tabia ya anasa inayoporomosha kiwango chake.

Mapema wiki hii, Mtalianao huyo alisema: "Andy anahitaji kuwa makini. Sijui chochote kuhusu aina hii ya maisha, ni matatizo binafsi ambayo siwezi kuyazungumzia.

"Ila kama anahitaji kuwa mchezaji mzuri na mwanamichezo, anahitaji apunguze kupunguza kunywa, hayupo kwenye kiwango chake cha juu kwa sasa."

Ila Dalglish ambaye alitumia kiasi cha £35m mwezi January alimtetea kwa kusema, "kwetu sisi tumezungumza mara kadhaa, ila imeangukia kwenye sikio la kiziwi, Andy hakuwa fiti kiasi cha kutosha msimu uliopita sababu ya majeraha,'' alisema meneja huyo.

"Tumeridhishwa na kiwango cha ufiti wake kwa mwaka huu, sababu ameondokana na majeraha yaliyokuwa yanamkabili."

"Haufahamu maisha yake, nani anafahamu maisha yake? Andy, nadhani ni mtu mwenye hekima zaidi ya watu wengi sana, na sidhani mwenendo wa maisha wake si kitu pale wanapotaka kuandika habari zao.

"Nadhani anashukuru ushauri wa Fabio Capello, na anamuheshimu sana Fabio Capello - na naamini pia Fabio Capello anamuheshimu sana Andy Carroll.''

Mancini aeleza sababu ya kumsajili Hargreaves

Roberto Mancini

Meneja wa Timu ya Manchester City Roberto Mancini, amesema mwanzoni nia yake kuu ilikuwa ni kumsajili mchezaji wa Roma Daniele de Rossi au mchezaji wa  Real Madrid Fernando Gago - ila akasema sababu za kifedha ndizo zilizosababisha amsajili Owen Hargreaves.

Mancini aliieleza the Independent: "Gago ndiye mchezaji tuliyemtaka kwa udi na uvumba, hatukutaka tutumie hela zaidi ya ile tuliyoipanga.

"De Rossi ni mmoja kati ya viungo wazuri hapa Duniani, ila siamini kama anaweza kuondoka Roma. Kwa hiyo kwenye kiungo tukaamua kumsajili  Hargreaves, ambaye yuko nje ya mkataba.''

Chelsea: Hatumuhitaji Modric tena

Andre Villas-Boas

Kocha wa Timu ya Chelsea Mreno Andre Villas-Boas, amesema baada ya kumsajili aliyekuwa kiungo wa timu ya Liverpool Raul Meireles, hatomuhitaji tena mchezaji aliyekuwa anamtaka kwa kipindi kirefu, kiungo mchezeshaji wa timu ya Tottenham Hotspur Luka Modric.

Alipoulizwa kama Chelsea watarudi na kumsajili tena mchezaji huyo wa Tottenham katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo mwezi January, Villas-Boas alisema: "Hapana, sidhani. Soko limeshafungwa na siwezi bashiri kitakachotokea mwezi January."

Vile vile kocha huyo, Villas-Boas amesikitishwa kwa kushindwa kumsajili beki wa kushoto toka Uruguay Alvaro Pereira, ambaye anakipiga na Klabu ya Porto.

"Tulikuwa mbali kuweza kufikia kiwango cha matakwa ya Porto kwa mchezaji huyo. Niko na furaha nikiwa na Ashley Cole na Ryan Bertrand."

Wakati huo huo, Didier Drogba, anakimbizana na muda kuweza kuwa fiti ili aweze kuwemo kwenye mechi ambayo Chelsea watacheza na Manchester United.

Kocha wa Blues Andre Villas-Boas amesema, mshambuliaji huyo atakosa mechi ya Jumamosi hii dhidi ya Sunderland, na ile ya Jumanne ya Kombe la Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Bayer Leverkusen.

Wednesday, September 7, 2011

Ferguson: Sneijder si wakufananishwa na Scholes

Xavi & Paul Scholes

KOCHA wa Klabu ya Manchester United Sir Alex Ferguson, amesema Wesley Sneijder asingeweza kuwa mtu sahihi kama mtu mbadala wa kumrithi Paul Scholes ndani ya Manchester United, huku akisisitiza ni wachezaji wa Barcelona pekee yaani Xavi na Andres Iniesta ndio umbao ungeweza kuwafananisha na mchezaji huyo na kiungo wa zamani wa Uingereza.
"Sneijder si aina ya mchezaji anayeweza kuwa mbadala wa Scholes," Ferguson alisema.

"Ni mchezaji mzuri, lakini hakuwa aina ya mchezaji tuliyekuwa tunamtafuta kuweza kumrith Scholes. Ni Xavi na Iniesta pekee ndio unaoweza kuwalinganisha na Scholes."

Hispania 6-0 Liechtenstein

Alvaro Negredo

Timu Taifa ya Hispania imeweza kupata ushindi wa 6-0 dhidi ya Liechtenstein.

David Villa aliingia wavuni mara mbili, Negredo naye akapiga bao mbili, huku Xavi na Sergio Ramos wakifunga goli moja moja.

Kwa ushindi huo Kikosi hicho cha Vicente Del Bosque, kimeweza fanikiwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la mataifa ya Ulaya, waikiwa wamejikusanyia pointi 18 kutokana na mechi 6 walizocheza, wakifatiwa na Czech Republic kwenye nafasi ya pili.

33′ Negredo
37′ Negredo
44′ Xavi
52′ Sergio Ramos
60′ David Villa
79′ David Villa

Ronaldinho Arudi na Kuanza kwa Ushindi

Ronaldinho kwenye mechi Brazil na Ghana

Kwenye mechi yake ya kwanza baada ya miezi  zaidi ya 10, Ronaldinho amerudi tena akiwa timu ya taifa ya Brazil, akianza mwanzo mwisho kuisaidia nchi yake kuishinda 1-0 dhidi ya Ghana.

Mabadiliko ya Ratiba VPL


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko madogo ya ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kutokana na Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid ulioko mkoani Arusha kuwa na shughuli nyingine za kijamii.
 
Kati ya Septemba 7 na 8 mwaka huu, na Septemba 17 na 18 mwaka huu, uwanja huo utatumika kwa shughuli za dini na mashindano ya riadha ya Safari International Marathon.

Mabadiliko ya ratiba yanahusisha mechi zifuatazo na tarehe mpya zikiwa katika mabano; Septemba 7 mwaka huu mechi namba 20- Oljoro JKT vs Azam (Septemba 9), Septemba 10 mwaka huu mechi namba 22- Azam vs Simba (Septemba 11), Septemba 11 mwaka huu mechi namba 26- Ruvu Shooting vs Yanga (Septemba 10).
 
Septemba 17 mwaka huu mechi namba 38- Oljoro JKT vs African Lyon (Septemba 19), Septemba 21 mwaka huu mechi namba 43- Kagera Sugar vs Oljoro JKT (Septemba 22), Septemba 21 mwaka huu mechi namba 49- Ruvu Shooting vs African Lyon (Septemba 20) na Septemba 24 mwaka huu mechi namba 54- Toto Africans vs Oljoro JKT (Septemba 25).

Mchezaji Bora wa Wiki Goal.com

Cesc Fabregas

Cesc Fabregas, wiki hii amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mtandao maarufu wa Goal

Jina: Francesc "Cesc" Fàbregas i Soler
Klabu: Barcelona
Nchi:Hispania
Miaka: 24
Nafasi: Kiungo

Mafanikio: Amesaidia ushindi kwa Barcelona na timu ya Taifa ya Hispania

Del Piero: Sijaamua hatma yangu

 Alessandro Del Piero

Mchezaji mkongwe wa Juventus Alessandro Del Piero, amesema bado hajaamua kama ataendelea kucheza mpira baada ya msimu huu wa 2011-12.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36, bado yupo kwenye mkataba unaomuweka mpaka mwezi June mwakani pale Turin, ila inaelezwa kwamba mwisho wa mkataba huo haimaanishi kwamba na yeye atastaafu baada ya msimu huu.

"Kufikiria juu ya mwisho wangu kwenye soka , si kitu ambacho kinanichukulia muda kuamua. Bado sijaamua kama huu utakuwa ni mwisho wangu kucheza na Juventus," Del Piero alieleza La Gazzetta dello Sport.

"Kufikiria juu ya kwamba huu ni mwaka wangu wa mwisho inanifanya nijitoe kwa zaidi ya asilimia 200, nahitaji kumaliza kipindi changu nikiwa kwenye mafanikio ya juu."

Nikijaribu kuangalia nyuma miaka 20 iliyopita, nitaangalia nikiwa nimeridhika sana."

Del Piero alianza kucheza kwenye kiwango cha juu akiwa KlabuPadova, ila akajiunga na Juventus mnamo 1993. Mchezaji huyo mpaka sasa ameweza kucheza jumla ya mechi 600 kwa timu hiyo ya Serie A na kuifungia jumla ya magoli 285.

Capello: Barcelona Watafungika

Fabio Capello

Kocha wa timu ya taifa ya Uingereza Fabio Capello amesema kwamba, anaamini haitachukua muda kwa timu kupata jibu juu ya aina ya mpira ambao timu ya Barcelona inaucheza.

Timu hiyo ya Catalans inaaminika na watu wengi kwamba ni timu kali ambayo haijawahi  tokea duniani, ila Capello anaamini kwamba utawala wao hautakuwa wa milele.

"Naweza kumuona mtu anayeweza kuizuia Barcelona kwa siku za mbele? Nafikiri ndio itawezekana, sababu tuna bahati kwamba tunaweza kuwasoma wapinzani," Capello alinikuliwa kwenye mtandao wa FIFA.

"Utapata ufumbuzi wa namna ya kuizuia Barcelona, kwa kuelewa uwezo wao. Utajifunza mengi, ukiangalia mchezo wao kwenye mikanda. Naamini baadhi ya timu zitapata dawa ya kuifunga."

Pia anaamini kwamba taratibu kama ilivyo asili ya mchezo, kiwango chao kinaweza kushuka.

Akaendelea kusema "Unapokuwa unashinda mara nyingi, wakati mwengine unakosa kitu kinachokufanya uwe makini kwa kila mchezo kuweza kushinda, wachezaji wengine pia wanazeeka kimchezo."

Barcelona wameshinda Kombe la mabingwa msimu uliopita, na wameanza msimu mpya wa2011-12, wakiwafunga wapinzani wao Real Madrid kwenye Supercop ya nchini kwao Hispania, wakaja kuwafunga Porto kwenye Supercup ya Ulaya.

Santos: Hakuna makubaliano ya Neymer kuuzwa

Neymer

Klabu ya Santos  ya nchini Brazil imesema haijafikia makubaliano na timu yoyote kumuuza mshambuliaji wake Neymar.

Klabu hiyo imetoa tamko hilo Jana Jumapili kwenye taarifa ndefu waliyoitoa kwenye Mtandao wake, taarifa hiyo imesisitiza kwamba hakuna dili yoyote ambayo wamefikia na Barcelona juu ya kumuhamisha mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19, ili aweze kuhamia Camp Nou ifikapo mwaka 2013.

"Kutokana na sababu binafsi zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni kuhusiana na Neymar, Santos Futebol Clube inapenda kutoa tamko rasmi kwamba, maelezo yanayotolewa na vyombo hivyo juu ya mustakabali wa Neymer sio za kweli” taarifa hiyo ilisema.

"Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu mara zote imekuwa na nia njema ya kuendelea kubaki na Neymer kwenye timu.”

Taarifa hiyo imekuja baada ya gazeti la Estadao siku ya Jumamosi kuandika kwamba, Santos na Barcelona wamefikia makubaliano ya awali kwa Neymar kujiunga na mabingwa Hispania na Ulaya baada ya miaka miwili toka sasa.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Bazil amekuwa akihusishwa na kuhamia Barcelona na kwa mahasimu wao Real Madrid katika kipindi cha majira ya joto, huku baadhi ya timu nyingine za Bara la Ulaya nazo zikihusishwa juu ya mpango huo.

Mara zote Neymer amekuwa akisisitiza kwamba kwa muda huu angependa kuendelea kucheza nchini mwake Brazil.